Alhamisi, 23 Aprili 2015

Kuomba

KUJIFUNZA KUWA WAKRISTO WAOMBAJI –LUKA 11:1 “BWANA, TUFUNDISHE SISI KUSALI”
Mpendwa katika Kristo Yesu,
Baada ya kujifunza somo la Kufunga na Kuomba nimeombwa kuingia kwa undani kidogo kwa habari ya uombaji. Wengine wanasema hawajui kuomba. Wengine wanasema wanajua kuomba lakini kwa kiwango kidogo sana. Wengine wanasema uombaji wao ni dakika 3 au 5 au 10 maneno yanawaishia!  Wengine wanasema wanataka nguvu ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya kuomba. Basi nakusihi fuatana nami tujifunze toka chini kabisa habari ya kuomba. Ukienda nami pamoja na kuamua kufanyia kazi mambo tutakayojifunza nakuhakikishia baada ya wiki 2 utaanza kuona matokeo tofauti katika uombaji wako. Roho Mtakatifu atakusaidia. Nyakati za nyuma nilikuwa siwezi kuingia kwenye maombi na kukaa katika uwepo wa Mungu kwa Zaidi ya dakika 20. Baada ya kujifunza kuomba (na bado naendelea kujifunza) nimekuja kujikuta saa moja kila napoingia kwenye maombi haitoshi hata kidogo. Nakumbuka miaka kadhaa nyuma niliingia katika maombi alfajiri. Kama baada ya dakika 20 nikawa nimemaliza kuomba kwa haraka zangu nikakimbilia kuanza kujiandaa kwa ajili ya kwenda kazini. Roho Mtakatifu akaniambia una mambo mengi ya kuomba lakini huna muda wa kukaa nami kwa utulivu kuomba. Una haraka na mambo yako kuliko kuomba. Nilijisikia vibaya sana. Nikamwambia Bwana wangu nisaidie. Kuanzia siku hiyo nikajipangia muda maalumu wa kutosha wa kuomba. Nimemuona Roho Mtakatifu akibadilisha maisha yangu ya kimwili na kiroho siku baada ya siku kwa kuwa nimedhamiria kuwa na ushirika naye anibadilishe kwa ajili ya kumtumikia yeye. Naendelea kujifunza siku baada ya siku.  Nami nikusihi ungana nami tujifunze jambo.
Mpendwa wangu nikuambie tu ukweli kwamba  Maombi ni ujuzi unaohitaji mazoezi ya kila siku. Hakuna ujuzi unaokaa kwa mtu pasipo mazoezi. Hata Roho Mtakatifu anasema kwa kinywa cha Mtume Paulo kwa habari ya utauwa kwamba  “..ujizoeze kupata utauwa” #1Tim 4:7. Kama kuna juhudi zozote tunaweza kuzifanya katika maisha yetu ya kimwili basi juhudi zenye matokeo mazuri ni pale tutakapofanya juhudi na mazoezi ya mambo ya kiroho. Si maandiko yanasema ‘Mtakatifu azidi kujitakasa’? Basi tujizoeze kujitakasa, tujizoeze kuomba, tujizoeze kufunga, tujizoeze kufanya kazi ya Mungu. Miili, na nafsi zetu zikizoea basi inakuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
Tusikae tusubiri muujiza wa jinsi ya kuwa waombaji wazuri ndugu zangu. Tusikae tusubiri muujiza wa kuwa walimu wazuri. Tusikae tusubiri muujiza wa kuwa Manabii wazuri. Tusikae tusubiri muujiza wa kuwa wainjilisti wazuri. Tusikae kusubiri muujiza wa kuwa wachungaji wazuri. Hakuna muujiza. Ukisikia wito wa Roho Mtakatifu inuka anza safari ya huo wito. Ni lazima tukae chini tufanye mazoezi haya ya kiroho. Na kwa kuwa Roho Mtakatifu mwenyewe ndiye anayetufundisha basi tukionyesha utayari huo atatufundisha nasi tutakuwa wazoefu na wenye kujaa nguvu na utaalamu katika maombi.
Fungu ambalo linabeba somo hili linalopatikana katika Luka 11:1 limebeba uzito usio wa kawaida. Wanafunzi wa Yesu wanamwambia ‘Bwana tufundishe sisi kusali’. Waliomba ombi hili maalumu si kwamba ndo ilikuwa siku ya kwanza au ya pili wamekutana na Bwana Yesu. Bali ilikuwa muda mrefu tu wakifanya kazi naye. Na ombi hili walilitoa maalumu baada ya kumuona Bwana Yesu akiomba. Ngoja nikusomeshe huu mstari mzima unavyosema ‘Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake’.
Ndugu yangu unaweza kujiuliza ni kipi mwanafunzi huyu aliona ni cha tofauti katika maombi ya Bwana Yesu? Unaweza kujiuliza hilo? Ni nini alikiona hasa hata akajiona wao hawajui kuomba? Yamkini aliyachunguza kwa undani sana maisha ya Bwana Yesu kila siku. Alikuwa hana muda wa kupumzika ovyo ovyo. Usiku atakesha kwenye maombi, asbh ataamka na uchovu hatasema ngoja nikapumzike bali ataendelea na kazi. Wakati ambapo wanafunzi watakuwa wamechoka yeye atajitenga nao ataenda kuomba. Hata nyakati zingine wakiwa katika kutembea kuelekea sehemu Fulani yeye katikati ya kutembea huko ataingia katika maombi. Utaona kwa kiwango gani wanafunzi waligundua maisha ya maombi jinsi alivyokuwa Bwana Yesu. Na kwa kuwa Kristo ni kipimo chetu, kanisa la leo haliwezi kuepuka kujifunza kutoka kwa Bwana Yesu kwa habari ya maisha ya maombi. Na Bwana Yesu alitoa ile wazungu wanaita ‘pattern’ ya maombi. Akatufundisha ile ambayo madhehebu mengi wanaiita SALA YA BWANA. Sala hii imebeba mambo mazito ambayo Mungu akitupa neema ya kuyapitia moja baada ya jingine Roho Mtakatifu atakusaidia kubadilika kwa kiwango kisichoneneka katika kuomba.
Mpendwa wangu kwa kujifunza somo hili nataka nikujengee ufahamu utakaokusaidia kuomba kwa Zaidi ya saa moja kila unapoingia katika maombi. Ujuzi huu kwa ujazo wa Roho Mtakatifu utasonga mbele na hakuna jambo gumu litakalosimama mbele yako utakaloshindwa kulisimamia katika maombi. Mpendwa wangu HAKUNA JAMBO LINASHINDIKANA KATIKA MAOMBI. Nimelithibitisha hilo. Ndo maana Bwana Yesu alithamini sana maombi. Hata Roho Mtakatifu asema kwa kinywa cha Paulo ‘“ombeni bila kukoma “1Thes 5:17
Pasipo kujali dhehebu lako nataka nikujengee msingi wa kuwa muombaji mwenye maarifa ya kiungu na nguvu za Roho Mtakatifu. Wengine wamekariri ili uwe mwombaji ni lazima ujiunge na dhehebu Fulani. Nakuhakikishia maadamu umemuamini Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako unayo nafasi ya kuwa mjuzi katika maombi kwani Roho Mtakatifu ndiye mwalimu wako. Sitaki ukariri mambo mpendwa wangu. Natamani ujifunze uwe na utaalamu binafsi na uzoefu wako binafsi na Mungu unayemtumikia jinsi atendavyo kazi katika maisha yako ya kila siku.
Labda nikuulize mpendwa wangu ni mara ngapi kwa siku tunaacha kula chakula??? Nadhani ni mara chache sana. Tena kuna wakristo wengine ukiwagusa kwenye suala la kuacha kula atakuona kama kichaa. Akigundua umefunga huli chakula kwa ajili ya maombi anakushangaa. Kwanini anashangaa, kwa sababu kula ni desturi ya kila siku ya mwanadamu. Kama ambavyo kila leo tunakula chakula hiki cha kimwili hadi tunakuwa na uzoefu wa vyakula tofauti tofauti je si Zaidi kujiwekea muda wa kuwa na maombi kila siku? Si vema mpendwa wangu ukajifunza kuomba kila siku kwa ajili ya kuutafuta uso wa Mungu maishani mwako? Au kwako haina maana yoyote kuwa karibu na Mungu katika maisha yako ya kila siku? Hutaki uongozi wa Mungu katika maisha yako binafsi ya kila siku? Hutaki uongozi wa Mungu katika masomo yako? Katika ndoa yako? Katika familia yenu? Katika jamii yenu? Katika kanisa lako? Katika Taifa lako? Huhitaji uongozi wa Mungu? Unataka nani akusaidie? Maana imeandikwa ‘Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata’  tena imeandikwa Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’. Sasa Mungu atakufundishaje kama uko mbali naye hutaki kusema naye katika maombi?
Kuna njia 3 tutazifuata zitakazotusadia kuwa na maarifa na nguvu ya kuomba
1. Kujitengea muda maalumu wa kuomba (itakusaidia ujue muda gani wa kuomba na kuwa na muda wa mara kwa mara kuomba)
2. Kuwa na orodha ya maombi ya kuombea (itakusaidia ujue kila unapoingia kuomba nini unaenda kuombea)
3. Kuwa na mahusiano mazuri na Mungu (Mahusiano na Mungu yatakusaidia kutaka kila wakati kuwa karibu na Mungu katika maombi)
Kwa leo nikomee hapa na tukikutana tutaangalia mkakati wa 1 wa jinsi ya kuomba. Mungu akubariki. Ukiwa una jambo lolote unataka kutushirikisha tuombe pamoja nawe basi wasilian
0653543333
Baba lightnes

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni