Jumanne, 14 Aprili 2015

Kuzaliwa mara ya pili

KUZALIWA MARA YA PILI NI UHUSIANO WAKO BINAFSI NA MUNGU
Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.  Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.  Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.  Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.  Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.  Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.  Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya? Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali.  Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni?   Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu.  Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;  ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye #YOH 3:1-15
Mpendwa katika Kristo Yesu nakusalimu katika jina la Yesu. Ndugu yangu kuna watu wanadhani kuzaliwa mara ya pili ama kuokoka  ni kwa sababu ya kuabudu kwenye dhehebu Fulani labda na kufuata mapokeo Fulani Fulani. Kuna watu wanadhani kuwa mshirika wa dhehebu Fulani na kuwa kiongozi labda au kuwa mkuu wa kitengo Fulani katika kundi Fulani kanisani ni tiketi ya kuokoka. Bwana Yesu anasema ‘Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu’. Hapa duniani hata mbinguni. Kama kanisa linaweza kuwa na mtu ambaye anajiita tu Askofu, Mchungaji, Nabii, Mtume, Padri, Shemasi au Mwinjilisti kwa kujiita tu bila kuzaliwa mara ya pili hakika hatauona ufalme wa Mungu.
Nilikuwa nikiongea na Mchungaji mmoja juzi akanisimulia habari ya ‘Mwinjilisti’ mmoja ambaye alikuwa mchawi maeneo fulani! Nilimuuliza mara mbili mbili mtu mchawi halafu kapewa ‘title’ ya kuwa Mwinjilisti Kanisani??! Akanambia ndivyo ilivyokuwa. Yule mtu aliwekwa kazini kama Mwinjilisti. Kazi yake akabaki kuroga waumini na kuleta kila aina ya migogoro kanisani! Nilishangaa, nikalishangaa kanisa alilokuwa akitumika na nikawashangaa waumini aliokuwa akiwachunga!
Mpendwa wangu kuzaliwa mara ya pili hakika ni mahusiano ya mtu binafsi na Mungu. Mazungumzo ya Bwana Yesu na Nikodemo yatatufunulia hakika ya kwamba mwanadamu aliyezaliwa kwa asili ya kibinadamu anapaswa kuzaliwa kwa asili ya kimbingu ili aweze kuurithi ufalme wa Mungu. ‘Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho’!
Mwanadamu alivyoanguka pale Edeni alipungukiwa na utukufu wa Mungu kwa kuwa kabla ya anguko aliumbwa kwa taswira na mfano wa Mungu. Asipofanywa upya ndani ya moyo wake na maisha kwa ujumla hawezi kamwe kuurithi ufalme wa Mbinguni. Na anafanywa upya kwa kutubu dhambi zake na kumwamini Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake naye aoshwe  dhambi zake na Roho Mtakatifu kwa damu ya Yesu na hivyo kuanza maisha mapya katika uhusiano wake na Roho Mtakatifu. Hili ni jambo la rohoni mpendwa lenye impact katika mwili. Sivyo kama wengine wanavyodhani. Wengine wanadhani ni kubatizwa kimwili. ‘Si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu #Tito 3:5. Kufanywa upya huku ndiko kunakoitwa ‘kuzaliwa mara ya pili’.
#Ezekiel 36:25-27 ‘Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.  Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda’
Kwanini kufanywa upya huku kuitwe kuzaliwa mara ya pili? Yamkini kama ambavyo kuzaliwa kwa kawaida kwa mwanadamu kulivyo, kwamba mtoto anapozaliwa, akianza kuivuta hewa hii duniani anatambulishwa na kuunganishwa na dunia hii. Ndivyo ilivyo na kuzaliwa kiroho kwamba tunatambulishwa na kuunganishwa katika ulimwengu wa Roho, tunaunganishwa maisha yetu na Roho na kuanza mahusiano na Mungu kwa roho zetu.
Kama ambavyo kuzaliwa kwa mwanadamu kimwili hufungua macho, masikio, na milango yote ya fahamu aweze kuona, kusikia, kuhisi n.k katika mambo yote ya kimwili vivyo hivyo tunapozaliwa katika roho tunafungua akili na fahamu zetu za rohoni tuone, tusikie na kuhisi vitu vya rohoni. Bwana Yesu anamuuliza Nikodemo ‘Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni (rohoni)? Paulo asema ‘Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.  Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, TUKIYAFASIRI MAMBO YA ROHONI KWA MANENO YA ROHONI.  Basi MWANADAMU WA TABIA YA ASILI HAYAPOKEI MAMBO YA ROHO WA MUNGU; MAANA KWAKE HUYO NI UPUZI, WALA HAWEZI KUYAFAHAMU, KWA KUWA YATAMBULIKANA KWA JINSI YA ROHONI. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu’.
Kuzaliwa kwa mwanadamu kimwili kunamleta duniani kufurahia kila kilicho chema katika dunia hii ambavyo kama asingezaliwa asingeweza kuvifurahia. Ndivyo ilivyo hata katika kuzaliwa katika roho tunaunganishwa na kufurahia maisha na vitu vya rohoni kama kufunuliwa kwa fahamu zetu kuijua kweli ya Mungu, kufanywa upya kwa mioyo yetu, kudhihirishwa kwa neema kuu ya wokovu wa Mungu kwetu, kupewa amani, furaha, upendo, kuwasiliana na Muumba Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo na Roho Mtakatifu aishie ndani yetu.
Kuzaliwa kimwili kwa mwanadamu humtambulisha mtu kwa wanadamu wenziwe. Katika kuenenda katika maisha atashirikiana na wanadamu hawa katika mambo mbali mbali. Katika tamaa zao, hofu zao, huzuni zao, kazi n.k Ndivyo ilivyo na katika maisha ya rohoni tunatambulishwa kwa Wakristo wenzetu na katika kuenenda tunashirikiana nao katika mambo mbalimbali kama furaha zao katika kumtumikia Mungu, kufanywa upya kwa rohoni , upendo ,  amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu n.k.
Tunapozaliwa katika mwili tunaanza kujifunza kupokea, kujaribu kula vyakula vya kutusaidia kukua na kuishi hapa duniani, vivyo hivyo tunapozaliwa kwa jinsi ya rohoni tunaanza kujenga hamu na kushiriki kunywa maziwa ya akili yasiyoghoshiwa yaani neno la Mungu kwa watoto wote wa Yesu kisha tunaanza kula chakula kigumu kama ‘nyama’ inayofaa kwa ajili ya kukua katika kumtumikia Mungu. Naam hata kukua katika wokovu huu mkuu wa Mungu aliye Hai na kuwa na maarifa ya rohoni, na uzoefu na utakatifu hadi kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, yaani Kristo kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo.
Je mpendwa wangu hutamani kukua hadi kufikia cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni